WAVUVI WAPEWA SIKU SABA KUREJEA KAZINI MARA MOJA
Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mwanza, ikiongozwa na Mkuu wa mkoa huo John Mongella, imewapa siku saba zaidi ya wavuvi 1,000 wa kisiwa cha Kasarazi wilayani Sengerema wanaoendelea na mgomo wa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria kurejea kazini mara moja, huku ikiwaonya vikali baadhi ya wavuvi wanaodaiwa kupanga njama za kuwatosa majini wamiliki wa Mitumbwi kutojaribu kufanya hivyo.
Mgogoro huo uliotangazwa na ITV mei 26 mwaka huu, hatimaye umetua
mikononi mwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella ambaye ameongozana na
kamati yake ya ulinzi na usalama hadi katika kijiji cha Kalebezyo,
halmashauri ya Buchosa kwa lengo la kusikiliza pande hizo mbili
zinazohasimiana, ambapo kila upande umeeleza malalamiko yake.
Kisha Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella akatoa msimamo wa
serikali kuhusu kauli za vitisho zinazodaiwa kutolewa na baadhi ya
wavuvi wa kisiwa hicho cha Kasarazi.
Mgogoro huo ulianza kufukuta mwezi aprili mwaka huu, baada ya
wamiliki wa vyombo vya uvuvi wapatao 150, waliowekeza katika kisiwa cha
Kasarazi kugundua kuwa wamekuwa wakipata hasara ya mamilioni ya shilingi
kutokana na hujuma ya mapato ya uvuvi wa dagaa pamoja na mafuta
inayodaiwa kufanywa na baadhi ya wavuvi wasio waaminifu.
Post a Comment